Monday, February 27, 2012

Acha wabunge wajiuzuru!


Spika: Nusu ya wabunge wanatamani kujiuzulu

Na Godfrey Mushi, Nipashe
27th February 2012


Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameibua upya mjadala wa posho za wabunge zilizokuwa zikidaiwa kupanda kutoka Sh. 70,000 hadi kufikia Sh. 230,000 kwa kila kikao anachohudhuria mbunge, akisema kuwa sakata hilo la nyongeza ya posho, limesababisha nusu ya wabunge kutishia kuachia ngazi kutokana na hali ngumu inayowakabili.

Spika Makinda alitoboa siri hiyo mwishoni mwa wiki mbele ya wakazi wa Jimbo la Njombe Kusini mkoani Iringa wakati akizumgumza nao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Ikwivaha, Njombe Mjini.

Alilazimika kuzungumzia sakata hilo baada ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kumtaka atoe ufafanuzi kuhusu suala la nyongeza ya posho za wabunge ambazo zimeibua mjadala na malumbano katika jamii nchini kwa miezi ya karibuni.

Aliyeibua suala la posho katika mkutano huo ni Ali Mhagama, ambaye alimtaka Spika Makinda, kueleza msimamo wake kuhusu posho za wabunge kwa kuwa yeye (Makinda) na Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, walinukuliwa wakiunga mkono nyongeza ya posho za wabunge.

“Mheshimiwa Spika, tunataka utueleze msimamo wako kuhusu posho za wabunge kwa sababu wewe na Samuel Sitta, mlikuwa mnaunga mkono nyongeza hizo,” alisema Mhagama.

Akijibu swali hilo, Spika Makinda alisema: “Kwa taarifa yako, mheshimiwa Mhagama, sasa hivi wabunge waliofika pale, nakwambia karibu nusu wanataka kuondoka ubunge, wanauliza mama tuache ubunge, nikasema hamuwezi kuacha mtasababisha hasara nyingine ya by-elections (chaguzi ndogo), wamechoka kabisa,hawakujua.”

Spika Makinda aliongeza: “Mimi nakwambia miaka 10 kuanzia sasa, mtu yeyote mwenye shughuli yake, ama aliyekuwa anafanya professional (taaluma) yake, hatagombea ubunge kwa sababu ni eneo la umaskini wa kutupwa kabisa…Aaah, mnapenda mnachopenda, lakini nawaambia facts (ukweli)! na mimi ni Mkristo kabisa, sisemi uongo.”

Aidha, Spika Makinda aliwataka wananchi hao kuelewa kuwa wabunge si watumishi wa serikali, bali ni kikundi cha watu ambao mkataba wao ni miaka mitano tu na wanayo sheria ya kwao peke yao ikiwamo sheria ya uendeshaji wa Bunge peke yake (Sheria namba 14 ya mwaka 2008) na kuongeza kuwa kuna Kamisheni ya kuhudumia wabunge ambayo imeundwa na mambo yake yaliyopo pale ni kimkataba tu.

Kufuatia hali hiyo, Spika Makinda, alilazimika pia kufafanua maslahi ya wabunge wanayopata ikiwamo mshahara wa Sh. milioni 2.3 kwa mwezi kabla ya kulipa kodi ya serikali.

Akifafanua kuhusu hilo, Spika Makinda, aliwaeleza wananchi hao kuwa kodi ya serikali ambayo mbunge anatakiwa kuilipa kwa mwezi ni zaidi ya Sh. 700,000.

“Hii posho tuliyokuwa tunaisema sisi tuna utaratibu wetu na duniani kote kuna taratibu za posho, tukamwongezea mbunge posho wakati wa vikao na ni siku tisa, vikao vyetu viko vinne ambapo vitatu ni siku tisa tisa, akirudi jimboni hapa kama mimi, hakuna cha allowance (posho) wala nini,” alifafanua Spika Makinda.

Tangu kuibuka kwa suala la nyongeza ya posho za wabunge wakati wa Mkutano wa Pili, makundi mbalimbali yalijitokeza na kupinga hoja zilizotolewa na wabunge kwamba wanataka nyongeza hiyo kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Wakati mjadala huo ukiendelea huku wananchi wengi wakipinga kuongezwa kwa posho kizo kwa maelezo kuwa sio wakati mwafaka kutokana na hali ngumu ya uchumi inayolikabili Taifa, Spika Makinda, alisema posho mpya zilikuwa zimeanza kulipwa.

Hata hivyo, kuna taarifa kuwa baada ya Rais Jakaya Kikwete, kulitaka Bunge kulitafakari upya suala la nyongeza ya posho, posho hizo zimesitishwa.

AOMBA KUNG’ATUKA UBUNGE

Katika hatua nyingine, Spika Makinda, alilazimika kuomba ridhaa ya wakazi wa Jimbo lake la Njombe Kusini, wamruhusu ang’atuke katika medani ya siasa baada ya muda wake kumalizika ifikapo mwaka 2015.

“Ninawaombeni mnikubalie ikifika 2015 nisigombee nimewatumikia kwa muda mrefu kwa hiyo na mimi nipumzike maana nataka kufanya shughuli zangu binafsi,” alisema Spika Makinda, akiwaomba wapiga kura wake.

Kabla Spika Makinda, hajawatangazia rasmi wapiga kura wake kwamba anataka kung’atuka ubunge, aliwahi kunukuliwa mara kadhaa akisema hana nia ya kugombea tena kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: